Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), ilifanya mkutano mkuu wa 35 ambao uliofanyika kwa siku nne katika Usharika wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili ulitoka na maazimio 36 na kuelezwa kuwa idadi ya Sharika katika Dayosisi hiyo imeongezeka kutoka 88 mwaka 2018 hadi 93 mwaka huu.

Maazimio hayo yametokana na Idara za Theolojia, Misioni na Uinjilisti ambayo ilikuwa na maazimio sita, Mipango na Fedha maazimio minane, Idara ya Huduma za Jamii maazimio matano na Idara ya Utawala, Utumishi na Milki ambayo ilikuwa na maazimio saba.

Maazimio mengine yalihusisha vituo vya Dayosisi hiyo vya Upendo Media Maazimio mawili, Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini, Dar es Salaam (TUDARCo), maazimio matatu na Maendeleo Bank maazimio matatu.

Mbali na kutoka na maazimio hayo, Mkutano huo ambao uliongozwa na Neno Kuu lenye kichwa kisemacho ‘Wote wawe na umoja kutoka kitabu cha Yohana 17: 21a, wajumbe walipata masomo kutoka Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana hapa nchini, Dk. Donald Mtetemela kwa siku zote nne, na pia kutoka kwa Mwalimu Christopher Mwakasege ambaye alifundisha kwa siku moja.

Askofu Mtetemela alifundisha juu ya umoja katika Kanisa na kueleza mambo kadhaa yanayovunja umoja na kueleza jinsi Kanisa linavyopaswa kuwa ili kudumisha umoja.

Mwl. Mwakasege alifundisha mambo sita ya kufanya ili kuwa na umoja lakini kila jambo likitakiwa kuanza kuwa na umoja katika maombi kwanza, kabla ya kuanza umoja wa kitu kingine.

Akifungua Mkutano huo, Dk Malasusa alisema kuwa DMP imeendelea kukua, kwani kwa sasa ina Sharika 93 ukilinganisha na Sharika 88 mwaka 2018/19. Vilevile alisema kuwa idadi ya Mitaa pia imeongezeka kutoka Mitaa 170 mwaka 2018/19 hadi Mitaa 186.