Wakristo wameshauriwa kuuanza mwaka mpya wa 2021 kwa kujiwekea malengo ya kiroho, kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye mambo mengine kila mwaka mpya unapoanza.

Ushauri huo umetolewa na Wachungaji wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Peter Chuma wa Usharika Mteule wa Kivule na Costantine Michael kutoka Usharika wa Mbagala jijini Dar es Salaam, wakati wakizungumza na UPENDO Media, Jumapili iliyopita kuhusu mambo ambayo Wakristo wanapaswa kuyafanya wakati mwaka mpya unapoanza.

Wachungaji hao walisema kuwa kuanza mwaka mpya ni neema na jambo la kumshukuru Mungu, hivyo wamtangulize na kuanza na yeye katika kila jambo ili ajifunue kwao kwa matendo yake makuu.

Wakati huohuo, Mch. Constantin amewasisitiza Washarika na Wakristo kwa jumla, kujifunza umuhimu wa kutoa sadaka ya Fungu la Kumi ili mambo ya msingi yanayotokana na sadaka hiyo yaambatane nao katika maisha yao.

Akihubiri katika Ibada iliyofanyika katika Usharika Mteule wa Kivule, Mch. Constantin alisema kuwa, utoaji ni shule ngumu kwa baadhi ya Wakristo kwa sababu ya kupenda kupokea kuliko kutoa.

Amesema kuwa kutokutoa kunasababisha umaskini kwa sababu asiyetoa hana cha kuvuna na pia haruhusu baraka za Mungu kwenye maisha yake.

Katika Ibada hiyo ya kwanza kwa mwaka huu, Washarika walitoa sadaka ya shukrani kwa matendo ambayo Mungu amewatendea akiwamo Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Peter Chuma ambaye alimshukuru Mungu kwa kutimiza umri wa miaka 60.