Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF), Askofu Dkt. Panti Philibus Musa na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Mchungaji Dkt. Martin Junge wameyaandikia Makanisa wanachama wa LWF wakiyashukuru kwa ushirikiano na kuwatakia kipindi chema cha majira ya Kwaresma.

Wakiangazia changamoto nyingi ambazo Washarika duniani kote wanakabiliana nazo tangu kuanza kwa ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona na hatua za kujitenga ambazo zimekuwa zikisisitizwa na wataalamu wa afya, viongozi hao wawili wa Kilutheri duniani wamesema katika kipindi hiki wanabaki kuwa wenye shukrani na wanatiwa moyo kwa jinsi Makanisa yanavyoitikia wito huo.

Wakitambua maisha ya wengi ambayo virusi vya ugonjwa huo vimeyachukua tangu mwaka uliopita, wamewasihi watu kuendelea kuwa macho na kuchukua tahadhari kwa umakini na wafuate ushauri wa mamlaka za umma.

Katika barua hiyo, Askofu Dkt. Musa na Mchungaji Dkt. Junge wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya usawa wa kupatikana kwa chanjo wakieleza kuwa Covid 19 imeonyesha na kufunua shida na tatizo la kimuundo wa usawa duniani.

Wameahidi kwamba LWF itaendeleza utetezi wa kupatikana kwa haki ya chanjo na usawa kwa wote na kuwahimiza viongozi wa Makanisa kufanya vivyo hivyo wakizingatia ukweli kwamba hakuna aliye salama, hadi watu wote watakapokuwa salama.