Kila mwaka Shirika la Open Doors hutoa ripoti ya hali ya mateso kwa Wakristo katika nchi zinazoipinga imani hiyo duniani.

Shirika hilo linatoa orodha ya nchi 50 ambazo ni vinara kwa mateso kwa Wakristo. Katika kipindi cha miaka 18, Korea Kaskazini imekuwa ikiongoza nchi hizo kwani ukatili wao unatisha.

Wapo Wakristo ambao wamezikwa wakiwa hai na wengine kuua kikatili kwa sababu tu ya kushikilia imani yao kwa Yesu Kristo. Ni kosa kubwa kuonekana na Biblia katika nchi hiyo na nyingine ambazo hazipendi kabisa kuusikia.

Hata hivyo, neema ya Mungu ni kubwa bado kuna Makanisa ya siri na Injili inahubiriwa japo kwa kificho. Nchi nyingine makanisa yemekuwa yakibomolewa na Wakristo wamekuwa wakilazimishwa kutundika picha za marais wa nchi hizo kwenye Makanisa na wanapokataa wanakuwa wamekikaribisha kifo.

Tukisoma kitabu cha Danieli pia tunaona namna ambavyo Danieli na wenzake walikutana na dhoruba za watawala ambao hawakupenda kabisa kuona Mungu anaabudiwa. Badala yake watawala walikuwa wakitaka sanamu zao ndizo ziabudiwe.

Hata hivyo, kina Danieli hawakuthubutu kusujudia sanamu za wafalme hao. Waliijua vema amri ya kwanza inayosema usiabudu Mungu mwingine ila mimi.

Ni rahisi kumuacha Mungu yanapokuja mambo magumu, lakini wapo Wakristo jasiri waliomtanguliza Mungu na wala hawatishwi na vitisho vyovyote.

Tunajua kuwa katika nchi hizo wapo ambao wamemwacha Kristo kwa sababu ya mateso hayo. Haya wanayokutana nayo wenzetu ni mazito, na hivyo tunapaswa kuitumia vema neema hii tuliyonayo.

Wakati sisi tukiwa huru kuabudu jinsi tupendavyo tutambue tu kuwa kuna wenzetu wanautamani uhuru tulionao lakini imekuwa vigumu kuupata.

Kuna Jumapili 52 tu kwa mwaka, lakini wapo Wakristo ambao hawaendi kabisa Kanisani. Zaidi sana wanaonekana siku za sikukuu, hii siyo sawa.

Tuwaombee wenzetu ambao wanaishi kwenye nchi hizo lakini tujue kwamba, kuishi kwenye nchi ambayo inaruhusu uhuru wa kuabudu ni neema kubwa.

Mkristo unamalizaje mwezi, mwaka hujasoma hata kitabu kimoja cha Biblia? Hujamwomba Mungu wala kumwabudu. Upo kwenye neema itumie.