Kwaresima imeanza, ni mwendo wa siku 40 za kuelekea Pasaka ambayo ni siku kubwa ya kielelezo cha wokovu wetu.

Tunapotaja Kwaresima, wengi wanajua kinachozungumziwa hata kama ni kwa kiwango kidogo, lakini si kila mtu anajali sana matukio yanayoambatana na majira haya ya Kwaresima. Moja ya matukio muhimu yanayoambatana na Kwaresima ni Ibada zinazofanyika kila Jumatano katika Makanisa yetu.

Ibada hizi zinabeba maana kubwa katika kuielewa Kwaresima, ni Ibada za kipekee kwa sababu hufanyika kipindi hiki tu katika mwaka.

Wengi wetu tunasubiri Ibada za Jumapili tu na Ibada kama hizi zakatikati ya juma si kitu kwetu, hali kama hii ndiyo inatufanya tusijue mambo mengi juu ya imani yetu licha ya kwamba tumezaliwa katika imani hiyo, tukabatizwa na kupata Kipaimara.

Tunakuwa Wakristo lakini tusiokuwa na mizizi, tupo kama yule mpanzi aliyepanda mbegu zake karibu na njia ambayo wapitanjia waliikanyaga au ndege waliila, hivyo haikuzaa kitu.

Tunakosea tunapokuwa tunashindwa kutoa kipaumbele kwenye mambo ya imani yetu kama haya lakini tunakuwa mstari wa mbele kusubiri sikukuu. Ili tukue kiroho lazima tukubali kutenga muda wa kwenda kwenye Ibada kama hizi katika kipindi hiki.

Jambo lolote linawezekana endapo tu utalipa kipaumbele. Lazima tuhakikishe kuwa tunakuwa na mizizi katika Ukristo na hapa ndipo imani inapothibitika, imani inathibitika inapokutana na mambo magumu, kinyume cha hapo tutakuwa kama yule mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga ambayo mvua iliponyesha na pepo zilipoipiga ilibomoka na kusombwa mbali.

Tunasombwa mbali kwa sababu hatutaki kuingia gharama za kuujua Ukristo kiundani, mfano mdogo ni Ibada hizi za Jumatano. Matokeo yake tunakuwa watu wa kupeperushwa na kila aina ya upepo unaokuja hasa katika nyakati hizi za mwisho ambazo kunaibuka imani za ajabu nyuma ya kivuli cha jina la Yesu.

Kumjua Mungu kunahitajika bidii pia, bidii katika kumtafuta. Tusikose Ibada.