Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo amesema Kanisa hilo linapaswa kufanya maboresho ya Ibada zake, lakini akasisitiza kuwa hatua hiyo lazima ichukuliwe bila kupotosha Neno la Mungu na taratibu nyingine za Kanisa hilo.

Katika salamu zake za Krismasi na Mwaka Mpya, Dkt Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, amesema: “Tutaboresha Ibada zetu kwa kuzingatia Neno la Mungu linafundishwa kikamilifu na kuutunza utambulisho wetu wa Kilutheri.”

“Nyakati hizi ni za uamsho, lazima kufuatiliwa kwa ukaribu mafundisho ya Neno la Mungu na usahihi wake. Pasipo ufuatiliaji Kanisa linaweza kuiga mitindo ya nje na kuacha kujiendesha kwa msingi wa Neno la Mungu bali kufuata watu,” alisema.

Alisema mabadiliko yoyote ambayo yanarahisisha utulivu wa Ibada kama kufungwa vifaa vya muziki vizuri, runinga, kurushwa matangazo kwa njia ya runinga na redio sio tatizo.

“Pamoja na hayo, Kanisa lazima lifuatilie na kuhakikisha neno linahubiriwa kwa usahihi na Ulutheri unatunzwa maana ndio ushuhuda wa Kanisa letu,” alisema Mkuu huyo wa KKKT.

Hata hivyo, Askofu Dkt. Shoo hakuweka wazi utaratibu utakaotumika kufanya maboresho hayo na iwapo yataingizwa rasmi katika miongozo ya Kanisa.

KKKT hutumia Kitabu cha Tumwabudu Mungu Wetu kama mwongozo mkuu wa Ibada zake mbalimbali. Kitabu hicho kinajumuisha nyimbo, litrujia na kalenda inayozingatia mwaka na majira ya Kanisa.