Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo ametoa salamu za Krismasi na mwaka mpya kutoka kitabu cha Mt.1:23, kinachosema; “Tazama bikira atachukua mimba. Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani Mungu pamoja nasi.

“Tunaadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Sikukuu hii ni muhimu sana kwetu sisi Wakristo, na kusema kweli kwa watu wote, kwa sababu ni habari njema inayohusu ukombozi wa wanadamu wote.

Anayezaliwa ni Mwana pekee wa Mungu. Yeye ameuacha utukufu wake mbinguni, azaliwe kama sisi na kuwa kama sisi ili apate kutuletea wokovu.

Tunasalimiana kwa maneno haya: Mwokozi amezaliwa, Haleluya! Yesu ndiye mwokozi wa ulimwengu, kuzaliwa kwake ni dhihirisho la kutimia kwa ahadi ya Mungu kuwa atamtuma mkombozi, atakayewaokoa watu na dhambi zao, na madhaifu yao yote.

Tunaiadhimisha sikukuu hii kwa furaha kwa sababu Yesu Kristo ni Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Mungu ameamua kuwa nasi kwa njia ya mwanawe. Kuzaliwa kwa Yesu kunaleta matumaini mapya kwa wote waliokata tamaa na kutembea gizani.

Kuzaliwa kwa Yesu ni dhihirisho kuwa Mungu anazijua hali zetu na mahangaiko yetu. Mungu anataka na kupenda kutuokoa. Mungu yu pamoja nasi wakati wote. Tukiwa na huyu Yesu tunao ushindi katika yote.

Tunaadhimisha Sikukuu ya mwaka huu tukiwa na matumaini tele, kuwa huyu Yesu aliyezaliwa atafanya jambo jipya katika maisha yetu, familia yetu, nchi yetu na dunia kwa ujumla kama tutampokea kweli na kumwamini.

Ninawatakia wote Sikukuu njema. Tusherehekee kwa upendo na amani, tukiwakumbuka wale walio na huzuni, nao tuwashirikishe furaha ya kuzaliwa kwa Mwokozi wetu." - Askofu Dkt. Fredrick Shoo