Kika mwezi Januari unapoanza watu hulalamika kwamba mwezi huo ni mgumu kutokana na mahitaji ya ada za shule, kodi za nyumba, kodi za biashara na mahitaji mengine kama hayo yakiwa mlangoni.

Wengine wameenda mbali kwa kusema kuwa mwezi huo unakuwa mrefu kutokana wengi wao kutokuwa na fedha huku mahitaji yakiwa hayana subira. Januari inatanguliwa na Desemba ambao una sherehe za Krismasi, Mwaka Mpya ambazo pia wengi huzitumia kusafiri kwenda makwao kwa ajili ya likizo lakini kujumuika na familia zao kusherehekea pamoja.

Zaidi ya hayo mwezi Desemba bei za vitu kama nguo, viatu hupanda na nauli za mabasi ya mikoani zote huwa juu mwezi huo. Sare za shule, madaftari nazo inapofika Januari hupanda bei. Kwa hiyo matumizi ya fedha kwa miezi hiyo miwili yanakuwa makubwa kuliko kawaida.

WACHUNGAJI

Mchungaji wa Dayosisi KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (DKMs), Godfrey Walalaze akizungumzia mtazamo wake kuhusu mwezi Januari alisema kuwa mwezi huo ni mwezi kama ilivyo miezi mingine, lakini unapewa majukumu makubwa na watu kutokana na kutokupangilia mambo.

Alisema kuwa hata katika masuala ya uzazi, mtoto wa kwanza ndiye mtoa dira au mwelekeo na kiongozi yeyote ndiye mtoa mwelekeo wa uongozi wa eneo husika, hivyo hata mwezi wa kwanza ndio ambao unatoa mwelekeo wa mwaka mzima.

“Kiroho mwezi wa kwanza ni lango, uzito wake ni kitu cha kwanza hivyo kila tunachopanga mwezi wa kwanza ni muhimu kukitafakari na kukisimamia ili kutoa mwanga wa kesho yako,” alisema Mch. Walalaze.

Mch. Elius Lugome wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani alisema kuwa tofauti kati ya Desemba na Januari itapatikana pale ambapo mtu ameamua kubadilisha mtindo wa kuishi kwa sababu miezi au tarehe zinakuwa namba tu kama hakuna badiliko la ndani kwa mtu.

“Kiroho mwezi Januari ni mwanzo wa majira mapya, katika ulimwengu wa roho mambo ni mapya kwa hiyo ipo haja ya kuwa na mipango madhubuti ya kuukabili mwezi Januari na kwa kufanya hivyo utapokea majira mapya kwa furaha.

“Ikumbukwe pia ili uweze kuona majira mapya, lazima nawe ubadilike na ubadilishe mtazamo wako wa kufikiri, kuenenda na kuishi kinyume na hivyo kila mwezi Januari ukifika utakuwa na malalamiko na huzuni zinazofanana,” alisema Mch. Lugome.

Mwalimu wa Neno la Mungu, Mhandisi Goodluck Mushi akizungumzia mtazamo wake kuhusu mwezi Januari alisema kuwa mwaka mpya ni majira mengine ambayo Mungu ameyaruhusu kwenye maisha, ambayo yanahitaji kutembea na uso wa Bwana, ili kufika pale ambapo Mungu amepakusudia.

“Januari ni mwezi ambao ni lango, hivyo kuwa makini na unachokipanga, mwezi wa kwanza ambao ni lango ambao unafungua ukurasa mpya wa mwaka,” alisema Mwalimu huyo wa Neno la Mungu.

Alisema imekuwa desturi ya kuubandika majukumu na uzito mwezi Januari kuliko kawaida. “Hakuna mwezi mbaya wala wa shida, kilichopo ni wewe kujipangilia tu, tunatangaza mwaka wa Bwana 2021 kwa jina la Yesu. “Tuache dhana ya ugumu wa Januari bali tutembee na ndoto ya Januari, Februari hadi Desemba juu ya kile tunachokipanga kwenye maisha ili kifanikiwe.

“Tukipoteza muda na Januari utashangaa mwezi huo umepita na majukumu umeyahamishia Februari, Februari nayo inapita majukumu unayahamishia Machi. Lazima uwe na mpango na ndoto kamilifu ya maisha ili Mungu akishuka kukubariki anabariki ndoto uliyonayo,” alisema.

Aliwataka watu kutotembea na uchungu wowote wala maumivu ya mwaka jana, bali watembee na walichojifunza mwaka jana.

Alifafanua kuwa kama mtu ataendelea kutembea na uchungu wa mwaka jana, hataona fursa za mwaka 2021 wala cha kujifunza.

MCHUMI

Profesa wa Uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema kuwa kiuchumi Januari imetanguliwa na matumizi mengi, kwani kabla mwezi huo haujafika kuna sikukuu mbalimbali ikiwamo Krismasi na Mwaka Mpya na kwa Wakristo kunakuwa na sherehe mbalimbali ikiwamo Kipaimara, Komunio na Ekaristi Takatifu.

“Hizi zote ni sherehe ambazo zinahitaji matumizi makubwa wakati kipato ni kilekile. “Ugumu unatokea kwa sababu matumizi yote hayo yanajikusanya mwisho wa mwaka na ni kipindi ambacho hata watoto wengi na wazazi pamoja na walezi wapo mapumziko ya mwisho wa mwaka,” alisema.

Profesa Ngowi alisema katika uchumi kuna kitu kinaitwa ‘Kusawazisha matumizi’ na anaeleza kuwa hiyo ni kanuni ambayo inalenga kuwa lazima ufahamu matumizi yako kulingana na kipato ulichonacho.

“Ulishajua Januari inakuja na kabla ya Januari inatanguliwa na Desemba ambayo ina mambo mengi ambayo unapaswa uyakabili.”

Alisema kinachopaswa kufanywa ni kusawazisha matumizi, “tunafahamu Desemba ikifika kuna Januari na Januari ikifika tutambue kuwa Desemba inakuja. “Kimsingi kwenye kanuni ya kusawazisha matumizi inahitaji kuweka akiba, ila vipato vyetu vingi havina uwezo wa kuweka akiba. Hii ndiyo changamoto kubwa, lakini tunapaswa kujitahidi kutunza na kuweka akiba kila mwezi, na ikishindikana basi kujiandaa tukijua wingi wa majukumu tuliyonayo Desemba ili Januari ikifika isiwe mzigo.”

WAZAZI

Mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, Maria George alisema mwezi Januari ni mgumu kwake kwa kuwa ana watoto wengi ambao wanasoma madarasa yaliyokaribiana.

“Nimepata changamoto mwezi huu kwa kuwa nina watoto wanne ambao wawili ni mapacha na wengine wamepishana miaka mitatu, mitatu. “Ada yao ni kubwa na mahitaji yao karibu yote yanafanana. Nimejitahidi kuwatengea bajeti yao lakini ninawiwa vigumu kwa sababu ya kipato changu,” alisema Maria.

Alisema kuwa tayari wameweka patano na mume wake juu ya kutunza watoto na majukumu ya nyumbani, lakini inakuwa changamoto kila mwaka kwa kuwa matumizi ni makubwa mno.

“Tumeamua kukopa kiasi cha fedha kuongezea pale tulipoweka akiba yetu kwa ajili ya kutimiza ndoto za watoto wetu. Kukopa kwetu kunatokana na kuweka akiba ambayo haijatosheleza kukidhi mahitaji,” alisema.

Naye Halima Hamisi mkazi wa Yombo jijini Dar es Salaam, alisema yeye ni mjane ambaye ni mjasiriamali na huwa kila akifanya kazi zake anajitahidi kuhakikisha kuwa watoto wake wawili wanasoma.

“Nacheza Vikoba na michezo ya mtaani ambayo kila siku tunatoa shilingi 2,000 na tukipokea mtu anapata shilingi 360,000. 

Hivyo nikipata hiyo hela huwa ninakimbilia kufanya matumizi ya shule ya watoto na nyingine naendeleza ujenzi wa nyumba yangu."

“Januari ni ngumu kwa kuwa maisha yetu ni tegemezi, wapo ndugu jamaa ambao wakati mwingine unakuta wanatutegemea,” aliongeza. Alisema mwezi Januari ni mgumu kwake maana kipato ni kidogo na hakitoshelezi mahitaji. “Tunaamua kujidhiki na kujitahidi kukimbizana na mahitaji ikiwemo kupunguza matumizi,” alisema.