Wakristo wametakiwa kutokwenda Kanisani kutafuta fedha, bali waende kumwabudu Mungu kwani fedha zinapatikana kwa kufanya kazi.

Rai hiyo ilitolewa na Mch. Enock Paulo wa Usharika wa Purana Dayosisi ya Kaskazini Kati, wakati akihubiri katika Ibada Jumapili iliyofanyika Mtaa wa Namelok uliopo Mirerani Mkoa wa Manyara.

Mch. Paulo alisema kuwa, watu wamekuwa wakitangatanga katika Makanisa ili kupata uchumi mzuri na kusahau kuwa fedha zinapatikana kwa kufanya kazi huku ukimtegemea Mungu lakini siyo kukimbia kimbia katika Makanisa mbalimbali ili kupata fedha.

“Yesu Kristo anawapenda bure, kinachotakiwa ni imani tu, utafanikiwa kwa kila unachokitaka lakini siyo mkubali kudanganywa kuwa kuna mahali mkienda mtapata fedha, mtahangaika mtakuja kugundua wakati mmeshapoteza muda mwingi wa kwenda katika Makanisa kutafuta fedha badala ya kumuabudu Mungu,” alisema Mch. Paulo.

Alieleza kuwa kwa kumwabudu Mungu, kulitii neno lake pamoja na kufanya kazi, inatosha kumfanya mtu afanikiwe na wala hakuhitaji msaada wa chumvi wala mafuta bali ni imani pekee na jitihada binafsi katika kufanya kazi kwa bidii.

Alifafanua kuwa Yesu alijitoa kuwa sadaka ya wanadamu na wanapaswa kutambua kuwa, wamekombolewa siyo kwa vitu vya muda mfupi bali kwa uzima wa milele kwa damu yake iliyomwagika msalabani.

“Damu ya Yesu iliyomwagika haipitwi na wakati wala haina mwisho, bali tunatakiwa kuweka gharama ya imani tu na imani hiyo inakuja kwa kulisikia Neno la Mungu na kukaa ndani yake,” alieleza.

Akihubiri kutoka kitabu cha Yeremia 1:12 na Waebrania 4:12, Mch. Paulo alifafanua kuwa, Neno la Mungu ni kila kitu katika maisha ya mtu na linapaswa kukaa kwa wingi kwani gharama ya wokovu imeshalipwa na kutimilika pale Yesu alipokufa Msalabani.

Mch. Paulo alimshukuru Mungu kwa kuwapa neema ya mvua ambayo walimlilia awape kutokana na hali ya ukame iliyokuwa ikisababisha ng’ombe kukosa malisho.

“Hali ilikuwa mbaya lakini hivi sasa tumeuona mkono wa Mungu, mvua imenyesha na sasa majani yamenza kuota, ng’ombe watapata malisho lakini pia wanapata maji na kama mnavyojua hili lilikuwa tatizo kubwa kwani mzunguko wa maisha yetu kwa asilimia kubwa yanategemea ng’ombe,” alieleza.