• "MUNGU ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku” Zaburi 7:11. Wakati wa utawala wa Sauli, Daudi alijipatia sifa nyingi. Sauli akawa na wivu akajaribu kumwua Daudi."

Mwanadamu ambaye moyoni mwake hamna neno la Mungu, ni ngumu sana kuzuia hasira yake.

Neno la Mungu linasema “Muwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi. Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia” Efe 4:26-29 Wakristo wameingia katika maisha mapya kwa sababu ya Ukombozi wa Yesu Kristo, na likumbukwe jambo hili tunaishi na watu wa dini mbalimbali, na wengine ambao hawamjui Mungu kabisa.

Wanadamu hawa wengine fikra zao zimetiwa giza hawamjali Mungu kabisa. Wakati Kanisa la Tanzania likimshukuru Mungu kwa neema na rehema zake, kutukinga na “Corona” Wapo wanaothubutu kumhuzunisha Mungu eti hana uwezo wa kuizuia “corona” sasa vilio ni dunia nzima, tujiulize sisi Kanisa la Tanzania, na Watanzania tunaingiaje mwaka wa 2021! Tunamshukuru Mungu namna gani, kwa wema wote aliotutendea? Na si kumshukuru Mungu tu, tunatakiwa kutambua kuwa tunaingia katika majira mapya, mambo ya zamani yameondoka, tuweke akili zetu katika mipango mipya, desturi mpya, mfano tabia za uvivu tuziache, kusema uongo tuache, badala yake tujijengee tabia ya kusema kweli siku zote.

Ni vizuri Wakristo wakawa na hasira juu ya dhambi, mawazo ya chuki na kisasi yakitokea, yaondolewe bila kukawia, ama sivyo, Shetani atatumia mwanya huo kutia udhaifu katika maisha yetu ya kiroho, mwili na nafsi. Wakati ule corona ilipotajwa kwa mara ya kwanza hapa Tanzania, watu walikuwa wasikivu kweli kweli! Tafiti mbalimbali za kimaabara zikafanywa, tunataka kuona mwaka 2021, tafiti hizo zikizaa matunda na kujitokeza hadharani kile kilichofanyiwa utafiti kikianza kutumika hapa nyumbani.

Vita vya corona Mungu ametushindia, na nchi yetu imeingia katika historia ya aina ya pekee, wakati tunakaribia kuuaga mwaka 2020, lazima tuwe wa kweli tukio la corona linaendelea kuyatesa mataifa makubwa duniani! Na limethibitika lile neno la Mungu lisemalo, Mungu huvitumia vitu dhaifu sana kuviaibisha vile vyenye nguvu kubwa, leo, tangawizi, limao, pilipili kichaa, asali asilia, vitunguu maji na vitu vingine asilia vina thamani kubwa hasa katika kuimalisha miili kupambana na magonjwa ikiwemo corona, sasa hivi nikitoa mfano mdogo limao linahitajika sana Kenya na linauzwa kwa bei ya juu, maana imethibitika linao uwezo kumsaidia mwanadamu katika mambo mbalimbali ikwemo corona.

Waliofanya tafiti, nawasihi jitokezeni hadharani tumtukuze Mungu, tumuaibishe Shetani na kazi zake.

Asipate nafasi tena kutuvuruga 2021. Ninao uhakika kuwa kuna kitu kipo katika maabara yetu kimeshafanyiwa utafiti kuwa kinaweza kabisa kupambana na covid 19! Sasa hivi kuna maneno ya chini kuwa chanjo iliyogunduliwa kule Marekani inaanza kutumika, lakini katika mitandao kunatokea maneno tofauti kutoka madaktari bingwa kuwa chanjo hiyo inahitaji kupewa muda zaidi wa majaribio kabla ya kutumika. Wanasema hivyo kwa sababu gani? Wanasema inaweza kuwa hatari kwa mwili wa mwanadamu, hii ina maana kuwa mwili utatawaliwa badala ya mwili kujitawala wenyewe! Chanjo hii inaweza kuua mfumo wa mwili kujikinga na maradhi, hivyo haifai.

Watanzania, Kanisa la Tanzania tuendelee kumwomba Mungu, wa neema, azidi kutupa hekima, maana tunaona na tunasikia kwa masikio, kuwa eti corona imechukua sura mpya, sisi tunasema Mungu tunayemwamini atabaki kuwa na nguvu zile zile, tunachotakiwa kukifanya sasa ni kuomba kwa bidii, kujitokeza kwa kuwaelimisha watu kuendelea kuwa na nidhamu, na usafi, kuzingatia maagizo ya wataalamu wetu, ile tujiepushe na hofu inayopenyezwa na adui.

Mungu ametupangia mpango wetu sisi Watanzania, tutabaki kumheshimu Mungu. Wapo watu kwa kuendekeza maslahi yao kwa hasira zao wanapenda kuona tunaharibikiwa, hawajui kuwa Mungu ana hasira pia, wapo wengi mwaka huu wa 2020, wamepatwa na matatizo mengi kutokana na hasira zao, afya zao zimeathirika.

Jambo moja la kusikitisha walipohalalisha hasira zao badala ya kutulia mbele za Mungu na kumuuliza wamejikuta katika mateso makubwa ya kutisha. Neno la Mungu wakati wote linajisimamia lenyewe. Lina kanuni kuhusu jinsi ya kushughulikia hasira kwa namna Mungu apendavyo, na jinsi ya kuzishinda hasira za dhambi.

Hasira sio dhambi kamwe. Hasira inayokupelekea kuacha jambo baya ni hasira nzuri, Neno la Mungu linasema “Koo lao ni kaburi wazi, kwa ndimi zao wametumia hila, Sumu ya fira i chini ya midomo yao.

Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu.” Warumi 3: 13-15. Mara nyingi umesikia watu wakidai haki. Mungu anasema hakuna mwenye haki hata mmoja. Watu wote katika hali yao ya asili ni watenda dhambi utu wao wote umeathirika vibaya na dhambi na unaegemea kuelekea kufanana na ulimwengu.

Mtu mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; bali mwenye hekima huizuia na kuituliza. Kamwe katika maisha yetu tusimchezee Mungu.

Mungu ni mwenye huruma, Yeye peke yake ndiye anayeona kila jambo na ndiye mtenda haki. Ikiwa Tanzania ni nchi ambayo inatajwa duniani kuwa iliwahi kuripoti corona na sasa haina ugonjwa huo, je! huo si muujiza tosha kuuthibitishia ulimwengu kuwa uwezo wa Mungu ni mkubwa!