Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo ameipongeza Dayosisi ya Magharibi Kati, Tabora kwa hatua kubwa ya kimaendeleo na Mipango mbalimbali waliyonayo licha ya kuwa Dayosisi changa katika Kanisa hilo ukilinganisha na Dayosisi nyingine.
 
Amesema hayo wakati akihubiri katika Ibada iliyofanyika KKKT, Dayosisi ya Magharibi Kati (Tabora) iliyoambatana na Uwekaji wa Jiwe la Msingi Ujenzi wa Jengo la Shule ya awali na msingi, harambee ya kuchangia Ujenzi huo pamoja na Uzinduzi wa Jengo la Saccos ya Dayosisi hiyo ambapo amesema hatua hiyo inatokana na kwenda pamoja na Yesu Kristo pamoja na Ushirikiano uliopo na taasisi nyingine.
 
Aidha katika kuelekea kipindi cha Kwaresma kinachoanza Jumatano ya Majivu Februari 17 Dkt. Shoo pamoja na kuwakumbusha Wakristo umuhimu wa kujinyenyekeza na kutubu.
 
Askofu wa Dayosisi hiyo Dkt. Isaac Kisiri Laisser akizungumza baada ya uzinduzi huo pamoja na kuwashukuru Viongozi mbalimbali walioshiriki katika tukio hilo muhimu amesema Saccos hiyo ina mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 15 hivyo amewaomba watu mbalimbali kunitumia Sacos hiyo kwa ajili ya kukuza vipato kwao.

Naye Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo anayemaliza muda wake Dkt. Greysin Nyadzi pamoja na na Mwenyekiti wa Saccos Monica Mlay pamoja na kuwashukuru Washarika kwa ushirikiano walioupata wameelezea hatua mbalimbali mpaka kufikia hatua hiyo.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Philemon Senga amesema Kanisa la KKKT na Makanisa mengine wameendelea kuwa na ushirikiano mkubwa sana na kwamba maendeleo ya Tanzania yatapatikana kwa kudumisha ushirikiano huo.
 
Katika Harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 150 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo ya shule.