Mwaka 2020 umeisha huku ukiacha kumbukumbu chungu na tamu. Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na homa kali ya mafua unaosababishwa na virusi vya corona (COVID 19) ndiyo uliotikisa mwaka huo.

Pia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 nao ni moja ya matukio ya kukumbukwa. Kuna misiba ya watu mashuhuri ambayo nayo pia iliacha vilio mwaka 2020.

Baadhi ya Maaskofu wa KKKT, wametoa tathmini yao kwa mwaka huo ulioisha na kuwaambia watu kuanza mambo yote ya mwaka 2021 na BWANA na kusahau mabaya yaliyopita. Wamekiri kuwa corona iliyumbisha imani za watu lakini hata hivyo Mungu alionekana kipindi chote ugonjwa huo ulipokuwa umeshika kasi.

Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki, Luka Mbedule alisema kuwa Covid 19 ilikuwa tishio na kama siyo Mungu, ugonjwa huo ulioanzia China ungeweza kuangamiza dunia nzima.

“Tulingia kwenye maisha magumu, hatusalimiani, tunavaa vitambaa, Ibada kusimama, taratibu za maisha zote zilibadilika hata kuzikana haikuwezekana. “Kwa kweli Mungu ametushindia kikamilifu kwa hili ashukuriwe na apewe sifa daima,” alisema.

Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Amoni Kinyunyu alisema kuwa mwaka 2020 umewaachia historia kutokana na Mungu kusimama na nchi hii katika uchaguzi mkuu na ugonjwa wa corona.

“Kwa matukio hayo mawili kwetu Bwana ni Ebeneza yaani hata sasa Bwana ametusaidia, wengi wanapitia machafuko makali wanapobadili viongozi lakini sisi amani imedumu na tuendelee kuidumisha,” alisema.

Askofu Mteule wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt. Msafiri Mbilu, alisema kuwa hatausahau mwaka 2020 kwa sababu ndiyo alichaguliwa kuwa Askofu wa Dayosisi hiyo. Mch. Dkt. Mbilu alichaguliwa kushika wadhifa huo mwezi Novemba na ataingizwa kazini katikati ya mwaka huu.

“2020 ni mwaka ambao mengi yamepita, COVID 19, uchaguzi mkuu. Nimeipokea Dayosisi yenye maendeleo kadhaa na vilevile changamoto kadha wa kadha ambazo ndizo tunaanza nazo kwa mwaka 2021, ni matumaini yetu kila jambo litakamilika kwa uweza wa Mungu Mwenyezi,” alisema.

Naye Askofu Dkt. Isaac Kissiri wa Dayosisi ya Magharibi Kati (Tabora), alisema kuwa corona imekatisha maisha ya watu lakini Mungu ameweka mkono wake katika hilo nalo limepita kwa utukufu wake. “Nafasi ya kipekee ni kumshukuru Mungu kwa kuwa ametushindia kikamilifu.

“Nawapongeza Wanadayosisi ya Magharibi Kati kwa namna ya kipekee walivyotoa ushirikiano kwa mwaka 2020, tuzidi kushirikiana mwaka 2021 ili Dayosisi izidi kupiga hatua moja zaidi,” alisema.

Akizungumzia mwaka 2021, Askofu Dkt. Kisiri alisema; “Lazima tuwe na moyo wa kumtumikia Mungu kikamilifu na kumtanguliza yeye, anza yote katika Bwana,” alisema. Alisema kuanza mwaka mpya ni sawa na kupanga bajeti ambayo huna hakika fedha utapata wapi au kwa ukamilifu gani.

“Kwa tumaini la Mungu, lazima tuwe na hakika ya kile tunachokitarajia, anza mwaka na Mungu ndoto zako zitakamilika,” alisema. Alisema katika mabadiliko ya miaka na nyakati lazima kujua kuwa hiyo ni misimu mipya, na yanahitajika mambo kadhaa ili kusonga mbele likiwamo la kumsikiliza Mungu katika kutimiza maono ili kile anachokitaka Mungu kitimie.

Askofu huyo aliongeza kuwa, kila mtu anatakiwa kujifanyia tathmini juu ya maisha yake binafsi ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kuacha mambo ya zamani na kupokea mambo mapya ili asiende kimazoea.

“Katika kujitathmini huko lazima tufanye kazi kwa bidii na juhudi kwa kutumia mazingira yetu yanayotuzunguka ili kujipatia kipato kwa ngazi ya mtu mmoja, mmoja hatimaye Taifa.”

Kwa upande mwingine, Dkt. Mbilu alizungumzia mipango ya Dayosisi ya Kaskazini Magharibi na kusema kuwa, mwaka mpya unawapa fursa ya kuanza upya. “Tutaanza kufufua kiwanda cha uchapishaji cha Vuga, kisha shule za sekondari Lwandai na Bangala. “Tutarekebisha kasoro zilizopo katika Chuo Kikuu cha SEKOMU ili usajili wake uendelee wa chuo kikuu.” Alisema kuwa wapo watu ambao wamekata tamaa na shule na vyuo vya Kanisa na vituo vya afya na kueleza kuwa tayari wamefanya marekebisho kadhaa, ikiwemo ya uendeshaji kwa lengo la kurejesha sifa na heshima yake ya awali.

Akizungumzia kuhudumia wananchi hasa Wanadayosisi, alisema tayari mipango kadhaa ya kuwainua kiuchumi imeanza kufanyiwa kazi na mwaka 2021 semina mbalimbali zitatolewa katika Sharika na Mitaa ambazo zitaibua fursa kulingana na mazingira ya watu wa eneo husika. “Uchumi wa mmoja, mmoja ukikua, familia inakua, Kanisa linakua na hatimaye Taifa linakua na kuimarika.”

Askofu Mbedule alisema mwaka 2021 lazima utazamwe kwa jicho jipya la tumaini. “Dayosisi yetu ya Kusini Mashariki, tumepanga kuendeleza mafundisho ya Neno la Mungu, mafundisho ya uchumi na kutambua fursa kwa lengo la kuinua vipato vya washarika na uwekezaji katika zao la korosho.”

Akizingumzia elimu alisema tayari mikakati ya uanzishwaji wa shule ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita imeanza. “Tumepanga kumkomboa Mwanadayosisi kiroho, kiakili na kiafya, hivyo mipango yetu mwaka huu ni kuhakikisha Dayosisi inasonga kivingine tofauti na nyuma.”

Askofu Kinyunyu akiizungumzia Dayosisi ya Dodoma, alisema mwaka 2021 hata katika Kalenda ya Kanisa inasema ni “Anza yote katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” ni hivyo hiyo ni ishara tosha kuwa mwaka huu lazima waishi tofauti na siyo kimazoea. Alisema pia ni wakati wa kuomba mvua ziwe za kiasi ili zisilete madhara.

“Tuendelee kutumia fursa iliyopo kwa serikali kuhamia Dodoma. Tunaendelea kufundisha watumishi na wenyeji wa Dodoma namna ya kukabili wingi wa watu na kuwa changamoto chanya ya kupiga hatua mpya zaidi ya maendeleo binafsi na ya Kanisa.”

Naye Askofu Dkt. Abednego Keshomshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi alisema, wanamshukuru Mungu kwa kuiwavusha kwenye corona. “Tunamshukuru Mungu tunapoingia 2021, tunapaswa kuwajibika kikamilifu na tusisahau kumwomnba Mungu kwa namna ambavyo tunapaswa kumwomba maana fadhili zake ni za milele.

Alitoa wito wa kuiombea serikali kwani ndiyo ilikuwa chachu ya kuomba kwa uhuru wakati ambao mataifa mengi yalikuwa yamefungia watu.

Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa wakati akihubiri katika Ibada ya Krismasi, Kanisa Kuu, Azania Front alisema kuwa Mungu ana upendo kwa wanadamu wanaoweka uhusiano mzuri kwake na kwamba ana uwezo wa kuwaondoa katika huzuni na changamoto mbalimbali zinazokatisha tamaa ikiwamo hofu na magonjwa.

Askofu huyo wa DMP alisisitiza umuhimu kwa Wakristo kumkaribisha Yesu azaliwe katika mioyo yao na kueleza kuwa sherehe haziwezi kuwa na maana kama Yesu hajazaliwa ndani ya moyo wako.

“Haijalishi unafanya kazi madhabahuni ama katika idara mbalimbali, kama hujawa karibu na Mungu hakika yote ufanyayo duniani ni bure, hivyo ni vema ukamkabidhi maisha yako ili ayatengeneze,” alisema.